MBUNGE wa Kigoma Kaskazini
(Chadema), Zitto Kabwe, ametajwa kuwa kichocheo cha kurejea kwa penzi la
vijana wenye umaarufu mkubwa nchini kwa sasa, Nasibu Abdu Juma
‘Diamond’ na Wema Isaac Sepetu.
Uwazi, lina mkanda wa video, unaowaonesha Diamond na Wema pamoja
kwa mara ya kwanza, baada ya muda mrefu wa kutupiana maneno mengi ya
kashfa, huku kila upande ukimshusha hadhi mwenzake.
Diamond na Wema,
walinaswa kwenye Tamasha la Kigoma All Stars, lililoandaliwa na Zitto
kisha kufanyika Julai 17, mwaka huu kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika,
Kigoma.
Shukurani kwa Zitto, kwani kupitia tamasha hilo, Diamond na
Wema, waliweza kudhihirisha kwa kila mtu kwamba uhusiano wao sasa
umerejea upya kwa kuambatana kimahaba ndani ya Mkoa wa Kigoma.
SAFARI ILIVYOKUWA TAMU Watu wengi wakijua kwamba
kuna uhasama mkubwa kati ya Wema na Diamond, Julai 17, mwaka huu,
ilikuwa ni mshangao wa aina yake kwa waliokuwepo Uwanja wa Ndege wa Mkoa
wa Kigoma, baada ya vijana hao kushuka wakiwa wameongozana.
Diamond akiwa amevaa shati jekundu na tai nyeusi, chini
akiondokea suruali ya jeans rangi ya bluu iliyopaushwa kimodo, huku Wema
akitokelezea kwa koti la rangi ya maziwa, ndani blauzi nyeusi, halafu
wote wameyaficha macho yao kwa miwani nyeusi, waliwaka vilivyo ndani ya
Ujiji, Kigoma.
Baada ya kuwasili Kigoma, Wema na Diamond walielekea
Hoteli ya Tanganyika Beach (ipo ufukweni mwa Ziwa Tanganyika) ambako
walipata pumziko walilohitaji kabla ya nyota huyo wa wimbo wa Mbagala,
hajaelekea Uwanja wa Lake Tanganyika kwenye Tamasha la Kigoma All Stars
a.k.a Leka Dutigite.
WEMA ALIFUATA NINI KIGOMA? Minong’ono ilitawala
kila kona ya Mkoa wa Kigoma kwamba Wema amekwenda kuwakilisha Leka
Dutigite, hivyo wakataraji kumuona Uwanja wa Lake Tanganyika, akitoa
sapoti yake kwenye tamasha hilo.
Wapo ambao waliacha shughuli zao
kwa ajili ya kwenda kumuona Wema tu uwanjani lakini waliambulia patupu,
kwani mrembo huyo hakuonekana kabisa.
Kutokana na hali hiyo, wale
waliovumisha stori kwamba Wema amekwenda Kigoma a.k.a Lwama, walionekana
wazushi wasiofaa kusikilizwa, bila kujua kwamba mtoto alijificha ndani
ya Hoteli ya Lake Tanganyika Beach.
HAKIKA WANAPENDANA Kama ukaribu wao
ulisababishwa na tamasha lililoandaliwa na Zitto peke yake, basi
wangekuwa na muonekano ‘feki’ sehemu chache wanazopita lakini kinyume
chake wao walithibitisha wanapendana haswaa!
Diamond, alishindwa kujichanganya na wasanii wenzake aliokuwa
nao kwenye shoo ya Kigoma kama akina Said Juma ‘Chegge’, Peter Msechu,
Banana Zorro, Mwasiti Almasi na wengineo, badala yake muda mwingi
aliutumia kuwa umbali wa mita sifuri kutoka alipo Wema.
‘Mtundu’ wa
nyimbo mbili mpaka sasa, Nai Nai na Baadaye, Omar Faraji Nyembo ‘Ommy
Dimpoz’, ndiye pekee aliyekuwa jirani na vijana hao maarufu, walioamua
kurejesha penzi lao kupitia mwavuli wa shoo hiyo.
Kwa upande mwingine, ni kama vile waliamua kwenda kufanya
tambiko nyumbani asili kwa mume mtarajiwa, yaani Diamond kwa sababu
chimbuko la Wema ni Mkoa wa Tabora, japo baba yake, Balozi Isaac Abraham
Sepetu, amejichimbia Zanzibar kwa miaka mingi.
Mtu mmoja, mwenye
hulka ya kutopitwa na mambo, akamueleza ripota wetu kuwa Julai 18,
wasanii hao walikwenda Hifadhi za Gombe na Mahale, mkoani humo lakini
jioni yake, Diamond aliongozana na Wema mpaka kwa babu yake, eneo la
Ujiji Posta, mkoani humo ambako walisomewa dua na Babu Nasibu.
RAHA NDANI YA TILAPIA HOTEL Safari ya furaha kwa
Wema na Diamond, ilihamia ndani ya Jiji la Miamba ya Mawe, Mwanza
‘Rocky City’ kwenye Hoteli ya Tilapia, iliyopo ufukweni mwa Ziwa
Victoria, eneo la Capri Point, hiyo ikiwa Julai 19, 2012.
Habari zinapasha kuwa wawili hao, walipumzika kwenye hoteli hiyo
kwa muda mfupi, wakati wanasubiri saa ya ndege yao ya kuwatoa Mwanza
hadi Dar es Salaam ifike.
Ndege waliyopanda Diamond na Wema kutoka Kigoma, ilitua Mwanza
saa 9:30 alasiri, hivyo kuanzia muda huo, waliutumia Tilapia Hotel mpaka
saa 2:30 usiku, wakaripoti Uwanja wa Ndege wa Jiji la Miamba ya Mawe,
kabla ya saa 3:50 usiku, usafiri huo wa anga, uliitupa mkono ardhi ya
Mwanza mpaka Dar es Salaam.
AIR PORT DAR ES SALAAM Mama mzazi wa Diamond,
Sanura Kassim ‘Sandra Sammi’, alionekana Uwanja wa Ndege wa Julius
Nyerere, kuanzia saa 4:45 usiku (Julai 19), hivyo kwa jicho la ripota
wetu, ikawa wazi kwamba amekwenda hapo kumpokea mwanaye kipenzi, Diamond
‘Sukari ya Warembo’.
Kutokana na safari hiyo kuwa mguu wa Diamond uliambatana na wa
Wema, kwenda kwenye shoo ya kutoa shukurani nyumbani kwao Kigoma, ni
wazi Mama Nasibu (Mama Diamond) alikuwa pale pia kwa minajili ya kumlaki
mkwe a.k.a Mka Mwana.
PW 415 YAWASILI DAR Diamond na Wema, walipanda
ndege ya Kampuni ya Precision Air, PW415 na ilipotimia saa 5:30 usiku,
ilitangazwa kuwa ndiyo inawasili kwenye uwanja huo wa ndege wenye jina
la muasisi wa taifa huru la Tanganyika na baadaye Tanzania, Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere ‘Baba wa Taifa’.
Milango ya saa 5:52,
Diamond na Wema, walipita kwenye mlango wa wanaowasili (arrivals gate),
wakiwa sambamba na Ommy Dimpoz, walipokelewa na Mama Nasibu hadi sehemu
ya maegesho ya magari uwanjani hapo.
Timu nzima, ilijipakia kwenye gari la Diamond aina Toyota Land Cruiser Prado, rangi ya fedha, wakatoweka eneo la uwanja huo.
DIAMOND KWA WASIWASI Saa 6:14 usiku (Julai 20),
Diamond alimpigia simu ripota wetu, eti akahoji kilichompeleka uwanja wa
ndege. Mahojiano yalikuwa hivi;
DIAMOND: Kiongozi nilikuona Air Port, pale ulikuwa unafanya nini?
RIPOTA: Aah, kumbe uliniona? Mlivyojikausha nikadhani hamkuniona. Kuna mzigo wangu nilikuwa naufuatilia pale.
DIAMOND: Mzigo wapi? Naomba uniambie ukweli.
RIPOTA:
Acha hizo dogo, unafikiri mimi nilikufuata wewe? Tena ningejua unafika
leo, halafu ujio wenyewe ni huo, ningetega kamera zangu na tuwapige
picha za kutosha.
DIAMOND: Aah, usifanye hivyo kiongozi.
Baada ya mazungumzo hayo, Diamond kila alipopigiwa simu hakupokea mpaka gazeti hili linanyanyuka kwenda kiwandani.
UFAFANUZI WA WEMA Wema alipopigiwa simu na
ripota wetu, alijibu kuwa yeye na Diamond hawajarudisha mapenzi,
isipokuwa hivi sasa wako karibu kama marafiki wazuri kwa ajili ya
kusaidiana mambo mbalimbali.
“Kusema ukweli kwa sasa sijafikiria kurejesha mapenzi na Diamond ila tupo karibu kama marafiki,” alisema Wema.
ZITTO NAYE Jitihada za kumpata Zitto aweze
kuzungumzia kurejea kwa penzi la Wema na Diamond kwenye tamasha
aliloliandaa, hazikuzaa matunda. Muda wote naibu huyo wa Kambi ya
Upinzania Bungeni, simu yake ilikuwa imezimwa.
WANANCHI WAMPONGEZA Fununu kuwa Wema na Diamond
wamerudiana zilivuma kwa kasi ndani ya mitandao ya kijamii na maoni ya
wengi yakaelekeza pongezi kwa Zitto, kwani kabla ya hapo, mastaa hao
walikuwa na uhasama mkubwa.
UNAKUMBUKA? Malumbano yao kwenye vyombo vya
habari? Diamond alipomfedhehesha Wema baada ya kukataa kupokea fedha
zake alizomtuza kwenye Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam Machi mwaka
huu? Je, kauli nzito za Mama Wema, Mariam Sepetu kwamba Diamond ni
kijana mbaya na hafai?
JIULIZE SASA Mpaka hapo bado unabisha kwamba
mapenzi ni upofu? Unaendelea kukataa kwamba mapenzi hayaulizwi kwa nini?
Diamond alipoachana Wema, alitua kwa Miss Tanzania namba mbili 2006-07,
Jokate Mwegelo, je, penzi lao limeyeyuka au bado lipo kwa sura gani?