INSIDE INAPATIKANA MADUKANI

FILAMU YA JADA ITAKUWA SOKONI 19.02.2015

JADA IPO SOKONI

JADA IPO SOKONI

Friday, March 6, 2015

ZA CHEMBE LAZIMA UKAE: TOP IN DAR INAKUWAJE TENA MZAZI?

KHALEED Mohamed, ni msanii wa muziki wa kizazi kipya mwenye uwezo usiotia shaka, kama utahitaji kujua kuhusu anachofanya. Na kama utasema utaje orodha ya wakongwe ambao bado wanatikisa katika ulimwengu wa Bongo Fleva ambao umetekwa na vijana, huwezi kumkosa katika watu wako Kumi Bora.


Msanii wa muziki wa kizazi kipya, Top In Dar au kifupi TID.

Top In Dar au kifupi TID ndilo jina lake maarufu la kisaniii, ingawa pia anafahamika kama Mnyama. Ukiniambia nikutajie majina ya wasanii wa Bongo wenye sauti nzuri na wanaojua kuzitumia, yeye yupo nambari za juujuu katika ubora. Cha kupendeza zaidi, hata akiwa jukwaani, anajua nini mashabiki wanahitaji kutoka kwake!

Orodha ya nyimbo zake kali ni ndefu pia na mafanikio yake kimuziki yanakufikisha hadi katika kilele cha ubora, miaka zaidi ya kumi tangu alipochomoza na kibao chake kilichomtambulisha cha Zeze. Nje ya muziki, TID ni mtoto wa mjini, tena wale wazawa wa Kinondoni, moja ya maeneo yanayosifika kwa vijana wake kujihusisha na mambo ya kihalifu, kama uvutaji bangi, unga, ubakaji na mengine yanayofanana na hayo.

Ndiyo maana haikushangaza wakati flani alipojikuta matatani kiasi cha kumfikisha jela, alikokaa kwa mwaka mmoja baada ya kutiwa hatiani kutokana na kitendo chake cha kumpiga mtu.

Nimewahi kuzungumza na TID katika safu hii siku za nyuma. Hii niliifanya, kama ninavyofanya mara zote kwa watu wote, kwa nia njema. ‘Mnyama’ ni mtu wangu wa karibu kikazi, nimefanya naye kwa muda wa kutosha kidogo na angalau ni kati ya wasanii ninaoweza kuwazungumzia.

Nimelazimika kurudi tena kusema naye hapa baada ya hivi karibuni mkongwe huyo kunukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari akiuponda wimbo mpya wa Ali Kiba uitwao Chekecha Cheketua ambao ameutoa hivi karibuni. Katika hali ambayo wapenda shari wanaweza kuita kebehi, TID alisema kibao hicho kitapotea ndani ya miezi mitatu!

Niseme wazi kuwa ninaheshimu sana maoni ya mtu juu ya kitu chochote kwa sababu ni haki yake iliyo ndani ya katiba yetu. Na ninaheshimu zaidi maoni hayo yakiwa hayakuandamana na matusi wala aina yoyote ya uhalifu, kama yalivyo ya msanii huyu nyota wa muda wote Bongo.

Tatizo langu linakuja tunapomtazama TID kama msanii mkubwa, ambaye pia kimuziki ni kama kaka wa Ali Kiba. Yes, kimuziki Kiba amekuja nyuma, akimkuta mwenzake tayari ni supastaa.

Ninafahamu kuwepo kwa kutokuelewana baina ya wasanii hawa wawili na wala sitaki kuingilia ugomvi wao kwa sababu sijui chanzo. Lakini tunapozungumzia kazi zao, siyo jambo linalopendeza mkongwe anapokebehi kazi ya mwenzake, ambaye kimsingi, alipaswa kumweleza kwa namna ambayo ingemuongezea kujiamini na hata kumheshimu mtoa mawazo.

Ni kama tunavyowaona wenzetu kule Ulaya, kwenye soka kwa mfano. Utakuta kesho ni mechi kubwa baina ya wapinzani, lakini leo wakizungumza na vyombo vya habari, kila upande unamsifia mwenzake, kwamba ni mzuri na lolote linaweza kutokea.

Katika kipindi ambacho muziki sasa umekuwa biashara, inayotaka mshikamano miongoni mwa wasanii wenyewe, sidhani kama ni jambo jema kuponda kazi ya mwenzako, kwa sababu kwanza unaharibu soko na kwa maana hiyo maisha ya mwenzako, lakini pia inaonyesha ni kwa kiwango gani sanaa imekosa umoja.

Hiyo ya kusema muziki gani huu, tuachiwe sisi mashabiki, ambao ndiyo walaji. Haitoi picha nzuri, wengine wanaweza kutafsiri kama ni wivu, jambo ambalo linamchafua zaidi TID na kumneemesha Kiba.

Ingekuwa mimi katika nafasi yake, ningeingia studio na kutoka na bonge la ngoma, halafu wakati wa utambulisho, naenda kuomba airtime nasema; “Watoto wadogo wanachafua biashara kwa ngoma za kitoto, nimekuja nayo hii kuwaonyesha nini maana ya muziki.”

No comments:

Post a Comment