Nilizaliwa tarehe 28 Januari 1974 mjini Singida, kwa Bi. Josephine Joseph na Bwana Yusuf Makamba. Mwaka 1978, nilipelekwa kuishi kijijini kwa bibi mzaa mama Kyaka, Kagera wakati mama ameenda kuendelea na masomo ya uuguzi. Kijijini kwetu ilikuwa umbali mfupi kutoka Mutukula, mpakani mwa Tanzania na Uganda. Idi Amini alipovamia Tanzania mwaka huo, kitongoji chetu kinachoitwa Kituntu, sio Kituntu ya Karagwe unayoijua wewe Padre, karibu na Kyaka nacho kilipigwa mabomu. Mimi na bibi yangu tulikimbia makazi yetu na kuhamia kwenye kambi ya wakimbizi eneo linaloitwa Mwisa. Baba yangu wakati huo alikuwa mstari wa mbele kwenye vita dhidi ya Idi Amin. Tulikaa kambini kwa muda baadaye tukafanyiwa utaratibu wa kuondoka kwenda Biharamulo na mama akaja kutuchukua. Sina kumbukumbu kubwa sana ya kipindi hiki kwa kuwa nilikuwa bado mdogo ila nakumbuka mvua nyingi, milio ya ndege na mabomu.
Nimesoma shule nne za msingi katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu kutokana na wazazi kuhamishwa mara kwa mara katika utumishi wa umma. Lakini pia kuanzia darasa la tatu hadi la tano nilirudishwa tena kijijini, Kituntu Kyaka, kukaa na bibi. Maisha ya kijijini siwezi kuyasahau. Enzi hizo, miaka ya mwanzoni mwa 1980, maisha ya kijijini yalikuwa magumu sana, bidhaa muhimu kama sukari, sabuni, dawa za mswaki, chumvi, na nyinginezo, zilikuwa adimu. Kutoka kitongojini Kituntu hadi shuleni ilikuwa mwendo mrefu na baada ya shule nilikuwa na kazi ya kwenda kuchunga mbuzi wa bibi, na baada ya kuchunga mbuzi kila jioni saa moja ilikuwa ni kazi ya kuchota maji mtoni, na baada ya hapo ilikuwa ni kumsaidia bibi kuuza pombe ya lubisi usiku na Jumamosi ilikuwa ni kwenda shamba kupalilia migomba na mikahawa. Maisha yale yalinifundisha mambo mengi. Baada ya miaka mitatu, nilirudi kukaa na wazazi na kumalizia darasa la saba Shule ya Msingi Masiwani, Tanga Mjini.
Nilianza Sekondari katika shule ya Sekondari Handeni, Tanga. Nakumbuka wakati naanza pale shule ile ilikuwa bado inajengwa, sisi tulikuwa Form 1 wa pili na ilikuwa haina tofauti kabisa na shule ambazo sasa zinaitwa shule za Kata. Kwa kuwa hii ilikuwa shule ya kutwa, mzazi wangu alipohamishwa kikazi kutoka Handeni, nikahamia Shule ya Sekondari Galanos Tanga, ambayo ilikuwa shule ya Serikali ya boarding.
Nilikuwa mwanafunzi mzuri pale Galanos, na, nikiwa kidato cha tatu, nikachaguliwa kuwa Makamu wa Kiranja Mkuu. Nilikuwa nafanya vizuri darasani, nikachagua mchepuo wa sayansi nikiwa na combination ya Chemistry (Kemia), Biology (Baiolojia) na Agriculture (Kilimo) (CBA). Nilipata daraja la kwanza kwenye mtihani wa kanda wa mock wa kidato cha nne, nikiwa na uhakika wa kuendelea na A-Level katika Shule ya Sekondari Kibaha, shule pekee iliyokuwa inafundisha mchepuo wa CBA hapa nchini. Hata hivyo, nilifanyiwa hujuma kubwa kutokana na siasa zinazomhusu Mzee wangu na kufutiwa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne.
Sikufa moyo, nilirudia mtihani kama mtahiniwa binafsi na kufaulu na kuweza kusoma A-Level katika Shule ya Sekondari Forest Hill Morogoro na nikapata Daraja la Pili kwenye mtihani wa Kidato cha Sita. Kabla ya kwenda Chuo Kikuu, niliamua kwenda kufanya kazi kwenye makambi ya wakimbizi kutoka Burundi yaliyokuwa wilaya ya Kasulu, Mkoani Kigoma. Niliipenda sana kazi ile ya kuhudumia wakimbizi na kuifanya kwa bidii kubwa. Nilipewa madaraka zaidi hadi kufikia nafasi ya Meneja wa Kambi Msaidizi wa Kambi ya Mtabila 2 iliyokuwa na wakimbizi zaidi la laki moja. Nilibahatika kuwa na wajibu na dhamana kubwa ya kuongoza kambi kubwa na wafanyakazi wengi nikiwa na umri mdogo tu wa miaka 21. Nilikuwa na wafanyakazi wengi, tena wengine watu wazima, waliokuwa wanaripoti kwangu. Nilikuwa na wajibu wa kuhakikisha kwamba wakimbizi laki moja wanapata viwanja vya kuishi, wanapata vifaa muhimu kama mahema, na wanapata chakula. Kazi ile ilibadilisha kabisa mtazamo wangu juu ya maisha. Baada ya kushuhudia adha wanayopata wanadamu wenzetu kutokana na vita hadi kukimbia makazi yao na nchi yao na kuja kukaa maporini kwenye nchi yetu, na baada ya kutafakari kuhusu udhalilishwaji na mateso yanayotokana na ukimbizi, niliamua kuachana na azma ya kusoma sayansi na uchumi na nikaamua kwamba maisha yangu nitayatoa katika kuchukua masomo kuhusu amani, na namna ya kutafuta amani ili nitoe mchango kwenye kuepusha vita na kupatikana kwa amani duniani. Hivyo, nilianza kutafuta vyuo duniani vinavyofundisha masuala ya amani. Nilipata chuo kimoja cha Wakatoliki Marekani, kinachoitwa St. John University. Lakini kilikuwa Chuo aghali kidogo, kwa hiyo nikaanza kusoma masomo ya awali kwenye Chuo kingine kidogo katika jiji la Boston kinachoitwa Quincy College na baadae nikajiunga na St. John University na kupata shahada ya kwanza ya sayansi ya masomo ya amani (Bachelor of Science in Peace Studies). Gharama za masomo zilikuwa kubwa na nilihangaika kufanya kazi mbalimbali, ikiwemo kazi za ulinzi na kuhudumia watu wenye magonjwa ya akili ili kulipia ada ya shule.
Baada ya kumaliza shahada ya kwanza, nilishinda tuzo ya kujiunga na taasisi ya Rais Mstaafu wa Marekani, Jimmy Carter, inayoitwa Carter Presidential Center iliyopo Atlanta hukohuko Marekani. Ilikuwa changamoto kubwa na fursa nzuri kwa sababu vijana wote waliojiunga pale walikuwa ni vijana mahiri sana na wenye uwezo mkubwa. Taasisi ile ilinipeleka nchini Sierra Leone kusimamia uchaguzi mkuu na kutekeleza mradi wa kufufua taasisi za haki zilizoporomoka baada ya vita. Nako pia nilijifunza mengi kuhusu ujenzi wa taifa.
Baada ya hapo nikaamua kuchukua shahada ya pili (Masters degree) kwenye Chuo Kikuu cha George Mason kilichoko Jimbo la Virginia, Marekani. Nilipata wakati mgumu kulipa ada, kiasi cha kukaribia kufukuzwa shule. Niliomba msaada kwa watu mbalimbali akiwemo Rais wa wakati ule Mhe. Benjamin William Mkapa. Bahati nzuri, alikubali kusaidia kwa sharti kwamba nije kutumia utaalamu wangu Serikalini nitakapomaliza masomo. Na ndivyo nilivyofanya. Baada ya masomo hayo, nikajiunga na Wizara ya Mambo ya Nje.
Mwaka 2005 nilifunga ndoa na mchumba wangu wa miaka minne, Ramona Urasa, na nimekuwa na familia yenye furaha sasa mwaka wa kumi. Pale Wizarani, nilipata fursa ya kufanya kazi na Waziri wa Mambo ya Nje wakati huo, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete. Nahisi alipenda kazi zangu na mara alipoamua kuwania nafasi ya Urais akanitaka nichukue likizo isiyo na malipo Serikalini ili niwe msaidizi wake kwenye kampeni zile. Siwezi kusahau maishani mwangu ile fursa kubwa kwani niliweza kuijua kwa kina nchi yangu na watu wake. Na kwa kuwa kampeni zinahusu ahadi za utatuzi wa kero za watu, nilipata fursa ya kujua kero za Watanzania kwenye kila wilaya ya nchi yetu.
Baada ya Rais Kikwete kushinda aliniteua kuwa Msaidizi wake Ikulu, nikiwa na jukumu la kumsaidia kuandika hotuba zake, pamoja na mambo mengine mengi ya uendeshaji wa shughuli zake za kila siku. Kazi ile ilikuwa ngumu kwa sababu inakulazimisha kujifunza na kujua karibu kila kitu ndani ya Serikali na duniani kwa ujumla, na kufanya utafiti karibu kila siku kwa sababu Rais anazungumza kila siku kuhusu mambo mbalimbali na kwa makundi mbalimbali. Pia kazi ile inakupa fursa ya kuhudhuria vikao vya Baraza la Mawaziri kama msikilizaji ambapo pia unajifunza mambo mengi ya uendeshaji wa Serikali, ikiwemo maamuzi muhimu ya kisera na kiutendaji yanavyofanywa. Ni nafasi ya heshima sana na sitamsahau Rais Kikwete kwa kunipa fursa ile.
Baba yangu alikuwa mwanasiasa karibu maisha yake yote lakini sikupata kuwaza kuingia kwenye siasa katika maisha yangu hadi nilipofanya kazi na Rais Kikwete. Baada ya kufanya kazi ile Ikulu kwa miaka mitano, nami nikahamasika na kuamua kushiriki katika uongozi wa umma. Niliamua kwenda kwetu Bumbuli kugombea nafasi ya Ubunge mwaka 2010, nikafanikiwa. Baada ya kuingia Bungeni nikapata nafasi ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini. Kazi ile tuliifanya vizuri sana na wenzangu kwenye Kamati hasa katika kipindi kile kigumu cha mgao wa umeme na matatizo ya mafuta nchini.
Baada ya kitambo kidogo, nikateuliwa kwenye Sekretarieti ya Chama nikiwa kama Katibu wa NEC wa Siasa na Mambo ya Nje, na nikawa Mjumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM. Nilishika nafasi hizi katika kipindi kigumu sana kisiasa kwa Chama chetu na nilijifunza mambo mengi na kutoa mchango wangu kwenye kukijenga na kukiimarisha. Baada ya kitambo kingine, nikateuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia.
Kuhusu kubebwa na jina la mzazi, kama nilivyosema hapo awali, pamoja na kwamba mzazi wangu alikuwa kwenye siasa kwa muda mrefu, binafsi, ingawa nilipenda na nilishiriki kuwa kiongozi tangu shuleni, sikuwa na mawazo ya kuingia katika siasa. Nilipokuwa Sekondari nilipenda kuwa mwanasayansi wa kilimo.
Baada ya kuzunguka nchi nzima kwenye kampeni ya 2005 na baada ya kufanya kazi ya kumsaidia Rais Ikulu ndipo nilipobaini kwamba siasa, ukiiendesha vizuri na kwa manufaa ya watu, inayo nafasi ya kubadilisha maisha ya watu. Nilipofanya uamuzi wa kugombea Ubunge, sikutaka ushauri wa baba yangu kwa sababu nilikuwa na uhakika kwamba angenikatalia. Niliamua mwenyewe na nikaanza harakati na ndipo nikamwambia. Kwa hiyo, unaweza kuwa na mzazi mwanasiasa na bado ukaweza kuwa na uhuru wa kujiamulia mwenyewe unataka kufanya nini.
Ni kweli kwamba jina maarufu la mzazi aliye kwenye siasa linasaidia kwa maana tayari kuna watu ambao wanamheshimu na ambao wapo tayari kukusaidia. Lakini pia jina hilohilo linaweza kukuharibia kwa sababu pia unaweza kurithi maadui zake, ambao wanakuona wewe ni sehemu ya yeye hata kama una mawazo na mtizamo huru. Kwa hiyo, siasa yangu nimejitahidi kuifanya kama mimi binafsi. Mimi na baba yangu tuna staili tofauti za siasa na mimi nina namna yangu ya kufanya mambo ambayo inatofautiana na yake. Lakini pia kuna mambo mengi mazuri ambayo nimejifunza kutoka kwake ikiwemo haja ya kuwa na msimamo usioyumba katika unayoyaamini na haja ya kutokumuogopa mtu yoyote.
No comments:
Post a Comment