INSIDE INAPATIKANA MADUKANI

FILAMU YA JADA ITAKUWA SOKONI 19.02.2015

JADA IPO SOKONI

JADA IPO SOKONI

Saturday, November 14, 2015

Filamu Ya Going Bongo Inahitaji Tuzo Zaidi: Mzee Chilo

Mwigizaji wa filamu, Chilo ametaja sababu tatu zinazoweza kuifanya filamu ya Going Bongo kushinda tuzo zaidi, ambazo ni maandalizi ya muda mrefu, kuona mbali na waigizaji kutambua kazi yao.
Mwigizaji huyo, ambaye jina lake halisi ni Ahmed Olutu, alisema inawezekana mambo mengine yamo ndani ya maandalizi, lakini kiuhalisia kila jambo linajitegemea, kwa sababu unaweza kuandaa kila kitu lakini waigizaji wakawa hawatambui thamani ya ulichokiandaa na kufanya mzaha katika kazi.
Chilo ni miongoni mwa wasanii walioigiza kwenye filamu ya Going Bongo iliyoshirikisha waigizaji kutoka nchi sita na ambayo imejishindia tuzo kadhaa.

Alisema maandalizi ya filamu hiyo yalikuwa ya hali ya juu tofauti na filamu nyingine nyingi alizoigiza kwa miaka 11 aliyokuwa kwenye tasnia hiyo ambayo alisema hufanyika siku moja kabla.
Alisema wakati wa upigaji picha wa filamu hiyo, hakukuwa na kukurupuka, kila kitu kilipangwa siku moja kabla utadhani kinafanyika wakati huo, huku wataalamu wa saikolojia wakimtayarisha mhusika kabla ya kuigiza kipande chake.
Chilo alisema mtunzi na mwigizaji mkuu wa filamu hiyo, Ernest Napoleon ana haki ya kushinda tuzo ya Ziff ya Mwigizaji Bora wa Ukanda wa Afrika Mashariki, kwa kuwa alijipanga na kutimiza lengo kwa zaidi ya asilimia 85.
Alisema ameigiza miaka mingi lakini katika filamu hiyo amejifunza mengi kama umakini kwa kila unachokifanya ili kizae matunda baadaye.
“Nafikiri Napoleon alikuwa anayatarajia haya ndiyo maana hakuna kilichokuwa kinajitokeza kwa bahati mbaya. Kila kitu kilipangwa, kila ulichouliza kilikuwa na majibu,” alisema Chilo.
Napoleon, ambaye pia ni muigizaji mkuu kwenye filamu hiyo, aliandika katika akaunti yake ya Twitter kuwa filamu hiyo imeshinda tuzo ya Beffta iliyotolewa nchini Uingereza kwenye kipengele cha Filamu Bora ya Kimataifa.
Mtanzania huyo anayeishi Marekani hajaridhika na ushindi wa tuzo hizo na ana mpango wa kuendelea kupambana kwenye tuzo nyingine kwa sababu anaamini ina kila sifa ya kushinda.
“Sikubahatisha, nilikuwa nina vitu vingi vya kufanya. Nilipopata wazo la kutayarisha filamu nilijipanga mwaka mzima hadi kuikamilisha. Nilitumia mwaka mmoja na nusu, hivyo naamini muda utajilipa kutokana na ubora wa kazi. Natarajia kushinda tuzo nyingi,” alisema.
Baadhi ya picha za filamu hiyo, inayoonyeshwa pia kupitia mtandao wa iTunes, zimechukuliwa nchini Tanzania.
Mmoja wa watayarishaji wa Going Bongo, Nick Marwa alisema kazi hiyo ni ya kwanza kushirikisha wataalamu kutoka nchi sita, ikiwamo Tanzania, Uingereza, Uturuki, Italia Kenya na Marekani.
Ilianza kurekodiwa jijini Los Angeles, Marekani na kumaliziwa Tanzania. Miongoni mwa wasanii walioigiza kwenye filamu hiyo ni Napoleon, Ashley Olds kutoka Marekani, Sauda Simba, Evance Bukuku na Ajmed Olutu kutoka Tanzania, Emanuella Galliusi kutoka Italia na Nyokabi Gethaiga kutoka Kenya.
Napoleon anasema gharama za utayarishaji zilifikia Sh450 milioni. Alisema mitaji midogo haiwezi kufanikisha kutoa filamu bora.
“Uwekezaji mkubwa unahitajika katika filamu,” alisema.
Chanzo: Mwananchi 

No comments:

Post a Comment