INSIDE INAPATIKANA MADUKANI

FILAMU YA JADA ITAKUWA SOKONI 19.02.2015

JADA IPO SOKONI

JADA IPO SOKONI

Thursday, October 18, 2012

WASANII LINDENI FARAGHA ZENU


Hivi karibuni kumeibuka mtindo wa wasanii wa kike na hata wa kiume kupata shutuma za aina mbali mbali ambazo nyingi kati ya hizo ziko kwenye mrengo wa maisha ya mtu ya ndani ambayo mara nyingi yanatakiwa kubaki kwa mtu mwenyewe.

Hapa tunamaanisha masuala yote yanayohusu faragha ya ndani kama masuala ya ndani ya kimahusiano, maadili, staha, utu na heshima ya mwili wa mtu au watu. Kwa bahati mbaya tangu masuala haya yameanza kuibuka hayapungui, bali yanazidi kuongezeka.

Kwa asilimia kubwa upande wa faragha ya matendo yanayohusiana na mahusiano na faragha ya viungo vya wahusika ndio vimekuwa ajenda kubwa katika vyombo vya habari. Matukio hayo yamekuwa si haba kujadiliwa katika mitandao ya kijamii pamoja na kurasa za magazeti mbali mbali karibu kila mwezi.

Tumeanza na maelezo hayo ili kujaribu kujadili yale yatokanayo na aina hii ya fedheha au kadhia ambayo imeonekana kwamba Watanzania wameanza kuichukia. Tutaanza na tukio la Diamond ambaye yeye alifanya kile kisichotarajiwa kwa kuonyesha nguo zake za ndani katika jukwaa la shoo ya Fiesta Dar-Es-Salaam kama ishara ya kuonyesha usafi wake.
Hapa cha kujiuliza je katika matendo yote ambayo Diamond angeweza kuyafanya ili kuiaminisha jamii juu ya usafi wake, hili la kuonyesha nguo za ndani ndio lilikuwa lenye umuhimu mkubwa kiasi cha kuamua kufanya hivyo? Je hakukuwa na aina nyingine ya kubainisha hilo?

Jambo lingine ambalo linakera zaidi ni namna wasanii wa kiume ambavyo wanapenda kuning’iza suruali ama kaptura zao (mlegezo). Wasanii hao wengi wao ni wale wa muziki wa kizazi kipya wamekuwa na tabia ambayo imekuwa inalalamikiwa sana ya kuvaa Jeans aina ya suruali na Kaptura chini ya makalio.

Narudi kwa dada zangu ambao wao ndio wanaonekana wahanga wakubwa wa matukio ya namna hii. Hatumaanishi kwamba tunataka kuwananga ama kuwasimanga, la hasha bali tunalotaka kushauri ni namna wasanii iwe wa muziki, filamu ama sanaa ambayo kwa namna moja ama nyingine inawafanya kuwa karibu na jamii.

Ni aibu kubwa kwa msanii kufanya jambo ambalo kwa maudhui yake kama hatakuwa na uwezo wa kulizuia lisidhuru heshima na haiba yake katika siku za usoni akaliruhusu lifanyike. Hapa tunamaanisha kwa mfano matumizi ya picha kwa kutumia aina yoyote ya camera iwe ya picha mgando ama zenye motion.

Ukiangalia kwa ndani mambo mengi ya namna hii hutokana na mazoea ambapo mtu huanza pole pole kwa kujipiga picha kisha akaziangalia mwenyewe. Baada ya hapo atapiga picha na kisha kuziangalia na wenzake mara nyingi huwa ni wale walioshibana wa jinsia moja.

Kisha tabia hiyo huanza kuenea kwenda kwa wapenzi wo. Hapa ndipo tatizo kubwa hutokea.
Shughuli ya faragha huanza kupungua kadiri siku zinavyokwenda ambapo mtu na rafiki zake huanza kuonyeshana picha hizo ambapo mpenzi wa kiume naye huanza kuwaonyesha maswahiba zake wa karibu na kisha kwa kutegemea uimara ama hatua ya uhusiano uliopo kati ya wahusika hao wote basi athari hujitokeza pale uhusiano huo baina ya watu hao utakapoharibika.
Upande mmoja wapo katika hali ya kukomoa ama kulipa kisasi huamua kuzisambaza kwa jamii kwa sababu anajua madhara ambayo yatamkuta mlengwa. Ushahidi wa hili lipo kwenye picha za mwanadada ambaye alishiriki video ya Masogange, Agnes.

Hatutaki kuingia kwa undani kuhusiana na suala hilo ila matokeo yake wote mnayajua.
Mwingine ambaye yamemkuta maswahibu ya namna hii ni pamoja na msanii wa muvi za kibongo Rayuu ambaye yeye kwa utashi wake ambao ni ngumu kuuelewa aliweka picha zake zikionyesha tattoo zilizoenea katika maeneo mbalimbali katika sehemu kubwa zaidi ya mwili wake, kitendo kilichoamsha majibizano makali kati yake na mdau mwingine wa tasnia ya filamu Sintah ambaye alihisi wao kama kina dada wamedhalilishwa na msichana mwenzao.

Pili uvaaji wa dada zetu ndio kichocheo kikubwa cha matatizo haya.Haiwezekani kwa akili ya kawaida tu mtu kuvaa nguo fupi isiyositiri faragha kwa asilimia 90 katika tafrija, sherehe ama shoo ya kijamii na kutegemea kwamba hali itakuwa shwari. Wema na Aunt Ezekiel ni mashuhuda wazuri katika hili.

Hatuna uhakika kama Aunt wakati analitolea utetezi suala hili alilifikiria kwa umakini wa hali ya juu na kusema waandishi wa habari wamekuwa wanawavizia chini ya jukwaa ili wawapige picha zitakazo onyshesha nguo za ndani.
Tunatambua kazi ya kueleimisha ama kuikosoa jamii ni ngumu lakini tunapenda kusema kwa hili itabidi dada zetu wabadilike kwani hawana ma jeans au nguo ndefu itakayofunika ugoko na kuondoa kadhia hiyo. Je ni lazima msanii avae nguo fupi sana kila wakati anapokuwa katika tafrija ya aina yeyote ile, ikiwemo na kwenye ku act?
Tunafikiri kama sio picha zile zilizowaonyesha Wema na Aunt Ezekiel namna ile, basi Jukwaa la fiesta jijini Dar-Es-Salaam lingekuwa na viroja kwani siku ile wengi wa wasanii walikuwa na tahadhari ya hali ya juu na kuamua kuvaa tofauti na hisia zao huwa zinavyowatuma.

Tulimwona jinsi Shilole alivyokuwa mwangalifu na hata ilimbidi kuvaa nguo ambayo ilimkwepesha na dhahama za picha chafu. Yeye pamoja na madensa wake walibadili aina ya nguo ambazo mara nyingi hutumia kwenye shoo zake.
Shilole akiwa jukwaani kwenye Fiesta Dar
Wasanii wanatakiwa watambue maana ya kudumisha uhusiano mzuri na jamii, usio na mikwaruzano ya ki itikadi, hisia, jinsia, dini, kabila wala fikra. Ingekuwa katika nchi nyingine tUnafikiri wasanii kama Diamond, Aunt Ezekiel na Wema sepetu wangepoteza nafasi zao za kibalozi kama wangekuwa nayo kama alivyo Diamond na ubalozi wa utalii.

Tunakumbushia tu…..Faragha ni kitu muhimu katika kulinda utu, kudumisha heshima na kustawisha maadili katika jamii.

Source: Vituko vya Mtaa

No comments:

Post a Comment