INSIDE INAPATIKANA MADUKANI

FILAMU YA JADA ITAKUWA SOKONI 19.02.2015

JADA IPO SOKONI

JADA IPO SOKONI

Wednesday, July 25, 2012

SAJUKI APATA GONJWA BAYA LAMSHAMBULIA UTI WA MGONGO

 

Sadick Juma Kilowoko ‘Sajuki’.
 
Sadick Juma Kilowoko ‘Sajuki’ akiwa na mkewe Wastara.

PAMOJA na kwamba afya ya staa wa filamu Bongo, Sadick Juma Kilowoko ‘Sajuki’ inaendelea vizuri, imegundulika kuwa ana ugonjwa mwingine tofauti na ule uliompeleka India kufanyiwa upasuaji,
Hivi karibuni, Sajuki alirejea kutoka nchini India alipokwenda kwa ajili ya matibabu ambapo alionekana kuwa na mabadiliko makubwa kiafya jambo lililowapa matumaini mashabiki wake.

HABARI MEZANI
Akizungumza na waandishi wetu, juzi, Jumapili nyumbani kwake, Tabata jijini Dar es Salaam, mke wa Sajuki, Wastara Juma alisema mumewe amegundulika kuwa na tatizo lingine walipokuwa nchini India kwa matibabu.
Alisema, hawakutaka kuweka hali hiyo mapema kwa Watanzania kwa kuhofia kusababisha simanzi, lakini sasa wanalazimika kufanya hivyo ili kuwafanya wajue kinachoendelea kwa staa wao.
“Kwa kweli mume wangu bado anaumwa na amegundulika kuwa na tatizo lingine ila tunamshukuru Mungu anaendelea vizuri,” alisema Wastara kwa huzuni nyingi.

NI UGONJWA GANI?
Kwa mujibu wa Wastara, walipokuwa India (katika Hospitali ya Apollo), Sajuki alifanyiwa vipimo mbalimbali ili kubaini matatizo yanayomsumbua ambapo aligundulika kuwa na tatizo kwenye uti wa mgongo na ngozi ya mwili mzima.
“Ana tatizo kwenye mfupa wa uti wa mgongo, lakini pia anasumbuliwa na tatizo jingine kwenye ngozi. Baada ya madaktari kugundua magonjwa hayo walimuanzishia dawa ya kutibu mgongo na mazoezi kwa ajili ya kumuweka sawa.
“Hizo dawa alianza kuzitumia tulipokuja huku, ambapo pia anaendelea na mazoezi. Tatizo lingine ni hilo la ngozi, ambalo pia anaendelea kutumia dawa,” alisema.

KWA NINI MGONGO?
Akifafanua kuhusu ugonjwa unaoshambulia sehemu ya mfupa wa uti wa mgongo, Wastara alisema madaktari walisema, tatizo hilo linasababishwa na kukaa kwa muda mrefu.
“Jambo hilo tulikubaliana nalo, kwa sababu ni kweli Sajuki huwa anakaa muda mrefu kwenye kompyuta kwa ajili ya kazi zake, lakini pia huwa anaendesha gari kwa muda mrefu. Tunaamini ndiyo chanzo cha ugonjwa huo kama madaktari walivyosema,” alisema na kuongeza:
“Lakini baada ya kupata dawa na ushauri  sasa anaendelea vizuri,  kwa sababu pia anafuata masharti aliyopewa vizuri. Huwa nahakikisha anapata muda mrefu wa kupumzika, hakai muda mwingi na haendeshi sana gari.
“Wamemwambia mambo mengi, hata kuinainama kila mara pia wamekataza. Kimsingi mwenzangu anahitaji uangalizi wa karibu sana. Hata hivyo anaweza kuendelea na filamu ila kwa kuzingatia na scene (onesho) yenyewe, ila kwa sasa anapumzika kwanza ili afya yake itengemae.”

KLINIKI KILA WIKI
Akiendelea kuzungumzia afya ya mumewe, Wastara alisema huwa wanalazimika kwenda Kliniki ya kila wiki katika hospitali moja jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuangaliwa maendeleo yake.
Aidha, alisema kila wiki tatu huwa wanatuma vipimo nchini India katika Hospitali ya Apollo aliyokuwa akitibiwa kwa lengo la kuchunguza maendeleo yake.

KUHUSU UGONJWA WA NGOZI
Wastara alisema, tatizo la ngozi alilonalo mumewe bado hajaanza kutumia dozi yake kwa sababu hawajapata fedha ya kutuma India ili waweze kutumiwa dawa zenyewe.
“Tupo kwenye mchakato wa kutafuta hizo fedha, lakini hali bado ni ngumu na anatakiwa kuanza dozi mapema kama madaktari walivyoshauri,” alisema na kuongeza:
“Mwezi Desemba (mwaka huu) anatakiwa kurudi tena ili aangaliwe tena maendeleo yake kwa ujumla. Yote hiyo ni gharama kubwa sana, lakini tunaamini Mungu atatusimamia.”

GHARAMA ZAMTOA CHOZI WASTARA
Alisema kwa namna mahitaji yalivyo mengi na yanayohitaji fedha, wapo kwenye wakati mgumu kuweza kuyakabili.
“Kiukweli bado tunahitaji msaada wa Watanzania wenzetu. Tunashukuru kwa wale waliojaliwa kutusaidia awali hadi kufanikisha safari yetu ya matibabu India lakini watakaoguswa wanaweza kuendelea kutusaidia.
“Mpaka sasa Sajuki hajaanza dozi ya ugonjwa wa ngozi na zipo nyingine anazotakiwa kuzitumia, lakini hazipatikani hapa...ni mpaka India.”

VIDUME VYAMTOKEA WASTARA
 Akizungumzia suala la usumbufu wa kimapenzi, Wastara alisema ni jambo la kawaida na ni kweli kuna baadhi ya wanaume wanatumia udhaifu wa ugonjwa wa mumewe kumshawishi kimapenzi.
“Kutongozwa ni jambo la kawaida kwa mwanamke, lakini mimi kama Wastara msimamo wangu ni kumheshimu mume wangu. Siwezi kushawishika kwa namna yoyote, kwanza hata hamu yenyewe sina.
“Ninachokiangalia kwa sasa ni afya ya mume wangu. Najua nina wajibu mkubwa wa kuhakikisha namhudumia mume wangu kwa mapenzi yote. Akili yangu haipo kwenye mapenzi kabisa, hali aliyonayo mume wangu inaniumiza sana.
“Kamwe sitamsaliti Sajuki wangu. Wema wake kwangu wakati nikiwa kwenye matatizo siwezi kuulipia kwa kumdhalilisha kwa kutoka na mwanaume mwingine eti kwa sababu anaumwa. Anayewaza kufanya hivyo, akajaribu kwingine, siyo kwangu.”

KALAMU YA MHARIRI
Kwa matatizo aliyonayo Sajuki ni wazi yeye na familia yake bado wanahitaji msaada wa hali na mali ili kuweza kukidhi mahitaji ya matibabu yanayomkabili kwa sasa.
Kama Mtanzania mwenzake, guswa na moyo wa utoaji na Mungu wa Mbinguni atakuongezea katika mifuko yako.
Ikiwa umeguswa, tafadhali tuma mchango wako kwenye akaunti namba 050000003047 yenye jina la Wastara Juma Issa iliyopo katika Benki ya Biashara ya Akiba (ACB) au tumia Tigopesa kwenda namba 0713 666113 yenye jina Wastara Juma.

No comments:

Post a Comment