Simon Mwakifamba
Jacob Steven ‘JB’
RAIS wa Shirikisho la Filamu Tanzania, Simon Mwakifamba, juzikati aliwapigia magoti wasanii wa Bongo Movie akijishusha na kuomba radhi kwa yote aliyokuwa akikwazana nao kabla ya kukaa chini na kuzungumza.
Tukio la kiongozi huyo kushusha goti chini kwa wasanii hao lilijiri Agosti 15, mwaka huu ndani ya Viwanja vya Leaders Club, Kinondoni jijini Dar es Salaam, mara baada ya Mwakifamba kuanza kuhutubia kikao kilichokuwa na lengo la wasanii kuungana kupinga wizi wa kazi zao.
Mwakifamba alisema kuwa umefikia wakati wake wa kujishusha ili kuifanya tasnia hiyo kuwa kitu kimoja na waweze kutimiza malengo yao.
MSIKILIZE JAMAA ALIVYOSHUKA
“Ndugu zangu na wasanii wenzangu, leo ni siku ya pekee ambapo nafarijika kwa kukutana na umati wa wasanii wenzangu wa tasnia hii ya filamu, hivyo basi kufuatia mambo mengi yaliyokuwepo baina yetu, leo napenda kuitambua rasmi Bongo Movie na kuomba radhi kwa yote mabaya niliyowahi kuyasema hapo nyuma.
“Baada ya kuomba radhi sasa nawaomba wasanii wote kuanzia leo hii tushikamane na tuweze kutokomeza wimbi la wizi wa kazi zetu,’ alisema Mwakifamba.
MWENYEKITI WA BONGO MOVIE ‘JB’ AMWONGELEA MWAKIFAMBA NJE YA JUKWAA
Akizungumzia kujirudi kwa Mwakifamba, Mwenyekiti wa Bongo Movie Club, Jacob Steven ‘JB’ alisema bosi mwenzake huyo amefanya jambo lenye heshima miongoni mwao na akasisitiza mshikamano baina yao kuanzia siku hiyo.
“Naweza kusema kuwa, Mwakifamba ameonesha jambo la heshima na kitendo chake cha kusema yaliyopita si ndwele tugange yajayo ni matokeo ya busara zake, tumempokea, tunaunga mkono mshikamano ili wasanii tupige hatua, tunataka kupambana na wezi wa kazi zetu,” alisema JB.
No comments:
Post a Comment