MASTAA ‘first class’ katika kiwanda cha filamu Bongo, Sylvia Shally na Coletha Raymond ‘Koleta’ wanadaiwa kukopa mawigi dukani na kuingia mitini.
Sakata hilo la aina yake limeibuliwa hivi karibuni ambapo Flora Mwande maarufu kwa jina la ‘Gari Kubwa’ mkazi wa Mbagala, Dar alisema anawadai kwa muda mrefu mastaa hao fedha za bidhaa mbalimbali yakiwemo mawigi.
Gari Kubwa alisema kuwa yeye ndiye anayewapendezesha mastaa hao kwa kuwakopesha nywele, pete, cheni na vitu vingine vya kike vyenye mvuto lakini mwisho wanampiga chenga kulipa fedha zake na kuingia mitini, jambo ambalo alidai limekuwa likimrudisha nyuma kimaendeleo.
“Sylvia alikuja dukani kwangu, Sayansi, Kijitonyama (Dar) Februari 17, 2011 akakopa nywele akisema yuko kwenye maandalizi ya kwenda nchini Nigeria. Alichukua ‘lesi wigi’ lenye thamani ya shilingi 150,000 lakini hajanilipa hadi leo. Mbaya zaidi hapokei simu yangu, inaniuma sana,” alisema Gari Kubwa.
Aliongeza: “Siyo huyo tu, Koleta naye alikuja kwangu Januari 5, 2011 na kukopa ‘lesi wigi’ na pete, vyote vikiwa na thamani ya shilingi 170,000. Hajalipa, nikimdai anasema eti simdai ina maana mimi sina akili timamu? Mimi mtu mzima najua ninachokifanya bwana.
“Wito wangu kwao aisee walipe fedha zangu, nitafurahi sana.”
Mwandishi wa gazeti hili alifunga safari mpaka nyumbani kwa Koleta, Makongo Juu, Dar na kusomewa mashitaka yake ambapo alifunguka:
“Katika maisha yangu naogopa sana dhuluma. Ni kweli Gari Kubwa ananidai shilingi 100,000, tatizo anaongeza fedha kila kukicha, mara anadai 170,000, mara 150,000. Mimi najua ilibaki 100,000 nitamlipa nikipona, si unajua kwa sasa naumwa?” alisema Koleta.
Akaongeza: “Halafu anakera sana huyo mama, ukikopa kitu kwake lazima akutangaze, siku moja Uwoya nilimuomba aniuzie cheni yake, nikawa nimesahau ATM kadi nyumbani, nikashangaa ananiambia nisimfanye kama alivyofanya Sylvia kwa Gari Kubwa, nikajua kumbe hata Sylvia anadaiwa.”
Paparazi wetu alimsaka Sylvia kwa simu zake za mkononi bila mafanikio. Jumatatu ya Agosti 20, 2012 akatumiwa meseji lakini hakujibu.
Jumanne ya Agosti 21, saa 3:30, 3:45 na 4:11 asubuhi Sylvia alipigiwa simu lakini pia hakupatikana.
No comments:
Post a Comment