Zari anatajwa kuwa ndiye mwanadada mzuri na mwenye mvuto zaidi Afrika Mashariki ambaye pia anashika namba moja kwa wanawake matajiri wa Uganda, akiongoza kwa kuingiza mshiko mrefu, kumiliki majumba na magari ya kifahari kama yale ya mastaa wa Kimarekani.
Zari amepata mafanikio makubwa katika muziki na kipindi chake cha The Boss Lady kwenye Runinga ya UBC nchini humo, kinachomuingizia mkwanja mrefu kutokana na matangazo kikifananishwa na kile cha mwanamitindo wa Marekani, Kim Kardashian cha Keep Up With The Kardashians.
Kwa mujibu wa Jarida la Times la Uganda, huenda Zari akaingia kwenye orodha ya wanawake matajiri zaidi Afrika siku chache zijazo endapo ataendelea kuzichanga.
Zari mwenye maskani yake Kampala na Afrika Kusini, anamiliki ndinga kibao za kisasa na zenye thamani kubwa kama BMW (2006) lenye thamani ya dola 47,000 (Sh. milioni 75.2), Black Chrysler (2008) linalouzwa dola 16,000 (Sh. milioni 25.6) na Audi Q7 (2010) linalogharimu dola 53,000 (Sh. milioni 84.8).
Mengine ni Silver Chrysler (2008) lenye thamani ya dola 13,000 (Sh. milioni 20.8), Jetta Volkswagen (2006) linalogharimu dola 27,000 (Sh. milioni 43.2), Mercedes Benz Convertible (2008) linalouzwa dola 26,000 (Sh. milioni 41.6), Range Rover Sport (2010) lenye thamani ya dola 109,000 (Sh. milioni 174.4), Lamborghini Gallardo (2010) linalogharimu dola 198,000 (Sh. milioni 316.8), Hummer H2 la dola 150,000 (Sh. milioni 240) na mengine mengi, yote yakiwa na jina lake badala ya namba za usajili.
Pia bidada huyo anamiliki maduka, hoteli na majumba ya kisasa kwenye miji mikubwa ya Pretoria na Cape Town nchini Afrika Kusini na Kampala, Uganda.
Lengo langu ni kutoa changamoto kwa mastaa wetu wanaotembelea magari ya kuazima, kukodisha au kuhongwa. Ipo mifano kibwena ya mastaa wa Kibongo wanaoishi kwa mizinga, kuhongwahongwa, ukuwadi lakini wenye mbwembwe na makeke mjini kumbe hawana lolote. Tujifunze kutoka kwa Zari!