MWIGIZAJI na mtayarishaji wa filamu za Swahiliwood, Jennifer Kyaka 'Odama', amefunguka kwa kusema kuwa anafanya kazi zake ikiwamo kuendesha kampuni ya J- Film 4 Life Production bila ya kumtegemea mwanaume yeyote.
Anasema yeye si mwanamke tegemezi kiasi cha kushindwa kutafuta fedha kwa ajili ya kuendesha mambo yake.
"Binafsi huwa sipendi kumtegemea wanaume, unajua kufanya hivyo mtu hutaweza kupiga hatua. Maendeleo yangu hayatokana na mwanaume, bali ni juhudi zangu," alisema.
"Huwa nafanya kazi kwa nguvu na kujituma zaidi ili kufikia malengo yangu, kuna changamoto nyingi sana katika kazi zetu hasa kwa mabinti.
"Ili usimame, ni lazima ujitoe kwa ajili ya kufanya kazi, natumia muda mwingi kuandaa filamu zangu lakini pia hata kazi za watu wengine ambao ni wateja wangu, sitaki kuwa tegemezi katika maisha yangu."
Odama alisema kuwa anajiona kuwa ni mwanamke jasiri kwani tangu afungue kampuni hiyo, tayari ana zaidi ya filamu 9 alizotengeneza. Kwake ni mafanikio makubwa.
Alisema pia kuwa kwa kutumia kampuni yake, amejipangia kwa mwaka mzima atengeneze filamu tano tu.
"Katika hizo najua pia nitakuwa nimetoa ajira kwa wasanii na watunzi wa miswada ya filamu za watu mbalimbali," alisema.
Source: http://syagalove.blogspot.com/2012/07/sitegemei-mwanaume-katika-kazi-zangu.html
No comments:
Post a Comment